Naibu gavana wa kaunti ya Kwale Bi Fatuma Achani, amemsuta Mbunge wa Kinango Benjamin Dalu Tayari, baada ya mbunge huyo kuibua madai kwamba amefuja shilingi bilioni 2 zilizotengewa mradi wa bwawa la Mwache.
Akiongea mjini Kinango Achani amesema kuwa maisha yake yako hatarini kufuatia matamshi ya chuki na uchochezi yaliyotolewa na mbunge huyo wa Kinango akisema kuwa ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kinango kuhusiana na suala hilo.
Ameyataja matamshi hayo kama propaganda, akisema kwamba ni njama ya kumharibia jina na azma yake ya kuwania kiti cha ugavana mwaka wa 2022.
Bi Achani amesisitiza kwamba siasa za uchochezi hazitayumbisha juhudi zake za kuwahudumia wakaazi wa Kwale, akisema ana haki ya kuzuru kila sehemu ya kaunti ya Kwale.
Mbunge wa Kinango Benjamin Dalu Tayari amedai kwamba Naibu gavana Fatuma Achani alifuja shilingi billion mbili zilizotengewa mradi wa bwawa la Mwache na kupeleka pesa hizo katika gatuzi dogo la Matuga na Msambweni.
Taarifa na Michael Otieno.