Story by Gabriel Mwaganjoni –
Maafisa wa idara ya upelelezi watazidi kumhoji Abubakar Amana, mkaazi wa kaunti ya Lamu anayedaiwa kutoa semi za chuki miongoni mwa kabila mbalimbali zinazoishi katika kaunti hiyo mwezi Disemba mwaka uliyopita.
Naibu kamanda mkuu wa polisi kanda ya Pwani Peter Njeru amesema wahusika tayari wanaendelea kumhoji Amana sawa na kukagua ukanda wa video uliyonakiliwa ukimuonyesha Amana akikashfu hali ya kaunti ya Lamu kufuatia kuongezeka kwa wageni katika kaunti hiyo.
Hata hivyo Mwanawe Abubakar, Rishad Amana aliyeandamana na Wakili Yusuf Abubakar na Mwenyekiti wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI Khelef Khalifa amesema Abubakar hakumchochea yeyote kupitia usemi wake.
Kwa upande wake, Khalifa ameikashfu idara ya usalama, afisi ya Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini sawa na Tume ya uiano na utangamano wa kitaifa NCIC kwa kuitekeleza sheria hiyo kiubaguzi.
Tayari Amana amejiwasilisha katika makao makuu ya polisi kanda ya Pwani, baada ya kuamrishwa kufanya hivyo kupitia barua ya Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Noordin Haji, aliyemtaka Inspekta mkuu wa polisi nchini Hillary Mutyambai kumchunguza Amana.