Kukithiri kwa ufisadi katika Idara ya usalama nchini kwa kiwango kikubwa kumehatarisha hali ya usalama wa taifa hili.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika linaloangazia maswala ya amani nchini ‘Kenya Community Support Centre’ Bi Phyllis Muema amesema kwamba hali ya ufisadi na ulafi wa mali miongoni mwa Maafisa wa usalama imedidimiza usalama wa nchi na ni lazima idara hiyo ipigwe msasa.
Akizungumza huko Kisauni Kaunti ya Mombasa, Bi Muema amesema kwamba hali imekuwa tata hasa katika idara ya utoaji vitambulisho huku wageni wakipata vitambulisho bila ya kukaguliwa kisha baadaye kutekeleza uhalifu na kuhatarisha maisha ya Wakenya.
Wakati uo huo Bi Muema anaikosoa jamii kwa kukumbata ufisadi badala ya kuripoti kwa idara husika ili wafisadi hao wakabiliwe akisema kwamba tabia ya Wakenya kuliona swala la ufsiadi kama la kawaida inahatarisha zaidi hali ya usalama wa nchi.