Rais Uhuru Kenyatta ameipongeza timu ya Taifa ya Soka Harambee Stars kwa kufuzu kuingia kwa michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika mwaka 2019.
Rais alisema kufuzu kwa timu ya Taifa kwa kinyanganyiro hicho barani kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 15 ni ufanisi wa kusisimua kwa wapenda soka nchini na akatoa hakikisho wa kuiunga mkono kikamilifu timu hiyo.
Thibitisho kwamba Timu ya Taifa Harambee Stars imefuzu kwa michuano hiyo ya Mataifa Bingwa Barani Afrika mwaka wa 2019 lilitangazwa siku ya Ijuma baada ya kikao kisicho cha kawaida cha siku nzima cha Kamati Kuu ya Shirikisho la kandanda Barani Afrika (CAF) Jijini Accra, Ghana, kubainisha uamuzi kuhusu timu ya taifa ya Sierra Leone.
Sierra Leone, ambayo ilikuwa katika kundi la F la kufuzu pamoja na Kenya, Ghana na Ethiopia haijashiriki michezo yake mitatu ya mwisho baada ya chama chake cha Soka kupigwa marufuku na Shirikisho la soka duniani FIFA.
Huku ikiwa imesalia mechi moja ya makundi kukamilika, Shirikisho la CAF liliafikia uamuzi wa kufutilia mbali matokeo yote yaliyohusisha taifa hilo la Afrika Magharibi na hivyo kuliacha kundi hilo na timu tatu pekee.
Sierra Leone ilikuwa imecheza tu mechi mbili katika kampeini yao na kwa sababu haikuwa imekamilisha nusu ya mechi zote za kufuzu, Shirikisho la CAF liliamua kufutilia mbali matokeo yote ya awali yaliyohusisha taifa hilo kulingana na kanuni za kufuzu.
Rais Kenyatta alisema Serikali kupitia Wizara ya Michezo itaendelea kuiunga mkono timu ya Taifa ya Soka inapojiandaa kwa kindumbwe-ndumbwe hicho Barani.