Elungata awahakikishia walimu na wanafunzi usalama wa kutosha
Story by Gabriel Mwaganjoni –
Idara ya usalama katika Ukanda wa Pwani imewahakikishia Walimu, Wanafunzi na Wazazi kwamba hali ya usalama imeimarishwa katika mazingira yote ambayo Wanafunzi watafanya mitihani yao ya kitaifa.
Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani John Elungata amesema swala la usalama limezingatiwa na mitihani hiyo itafanywa kulingana na ratba iliyowekwa.
Katika ziara yake katika kaunti ya Taita Taveta alikokagua makasha ya kuhifadhi mitihani, Elungata amesema mipangilio yote imekamilika.
Na kuhusu kaunti zinazokumbwa na utata wa kiusalama kama vile vile kaunti ya Lamu na Tana river, Afisa huyo tawala amekariri kwamba tayari amefanya ziara katika kaunti hizo mbili akiwa na lengo la kuweka mipangilio inayostahili kuhusu jinsi mtihani huo utakavyosambazwa vituoni.
Kulingana na Baraza kuu la mitihani nchini KNEC, jumla ya wanafunzi milioni 1,225,693 walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE unaoanza juma lijalo tarehe 7 Machi huku jumla ya wanafunzi 831,026 wakisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne KCSE uliyoanza siku ya Jumatatu katika masomo la lugha ya kigeni, huku mtihani rasmi wa nadharia na elimu zoezi ukianza tarehe 11 mwezi Machi hadi Aprili Mosi.