Serikali ya Uingereza kufanikisha ujenzi wa barabara ya Nyerere-Mbaraki kwa dola milioni 3.6
Story by Ali Chete-
Serikali ya kaunti ya Mombasa ikishirikiana na ubalozi wa Uingireza pamoja na kampuni ya kibinafsi ya Trademark East Africa inapania kuboresha miundo msingi katika kaunti hiyo.
Hii ni baada ya wadau wa maswala ya kibiashara kuzindua ujenzi wa barabara ya Nyerere – Mbaraki kutokea eneo la feri yenye urefu wa kilomita 1.2.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo, Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amesema barabara hiyo itaimarisha usafirishaji wa makasha kutoka bandari ya Mombasa hadi kampuni za kuhifadhi makashazilizoko eneo la Mbaraki.
Joho amesema mradi huo utabuni nafasi za ajira kwa vijana wa kaunti hiyo kwani mradi huo utagharimu serikali ya Uingereza dola milioni 3.6 na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari mwaka ujao.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Balozi wa Uingereza humu nchini Jane Marriott pamoja na Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Trademark East African Frank Matsaert ambao wamesema ujenzi huo utakapokamilika itakuwa ni afueni kubwa kwa wafanyabiashara.