Siasa za kinyang’anyiro cha ugavana wa Mombasa zazidi kupamba moto
Story by Gabriel Mwaganjoni –
Aliyekuwa Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba amemsihi mwanasiasa na mwekezaji Suleiman Shahbal aliyetangaza nia yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa kutowaachisha kazi wafanyakazi wanaohudumu katika Serikali ya kaunti hiyo.
Bedzimba amesema kuna baadhi ya wanasiasa wa kaunti hiyo waliotangaza kuwania kiti hicho wamekuwa wakitoa ilaani mapema kwamba pindi watakapoingia uongozini watawatimua kazini wahudumu wote wa Serikali hiyo.
Akizungumzia swala hilo, Mwanasiasa Suleiman Shahbal amewahakikishia wafanyakazi wote wa Serikali ya kaunti hiyo kwamba watasalia kazini pindi atakapoingia uongozini kama gavana wa Mombasa mwaka 2022.
Shahbal aliyekuwa akiwahutubia vijana katika eneo bunge la Kisauni amesema mbinu ya kuufufua uchumi wa kaunti ya Mombasa ni kubuni ajira kwa vijana na kuwaletea wawekezaji kutoka ughaibuni.
Kinyang’anyiro hicho cha ugavana wa Mombasa kimewavutia wanasiasa Suleiman Shahbal , Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo, aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar Sarai miongoni mwa wagombea wengine.