Kenya Airways imesitisha safari za ndege zake za kuelekea jiji la Mumbai
Kampuni ya ndege ya Kenya Airways imesitisha safari za ndege zake za kwenda na kurudi katika jiji la Mumbai nchini India kufuatia ongekezo la maambukizi ya virusi vya Corona nchini India.
Katika taarifa kwa vyombo ya habari, Kampuni hiyo imesema imechukua hatua hiyo baada ya serikali kupiga marufuku ndege za India kuingia humu nchini kwa kipindi cha siku 14 ili kudhibiti msambao wa virusi vya Corona.
Taarifa hiyo imesema inazingatia agizo la serikali la kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona huku ikiwaomba radhi abiria wake wanaolenga kusafari katika jiji hilo.
Hatua ya kampuni hiyo kusitisha safari za ndege zake kwa mda usiojulikana imetokana na baadhi ya mataifa ya Singapore, Bangladesh, Hongkong, na Uingereza kuungana na Kenya na kupiga marufuku safari za ndege kutoka nchini India.