Magavana wanasema vikwazo vilivyowekwa ni changamoto kwa serikali za kaunti
Picha kwa hisani –
Magavana wa humu nchini wamesema vikwazo vilivyowekwa na serikali ya kitaifa ni changamoto kuu kwa serikali za kaunti katika kutekeleza mpango wa afya kwa wote wa ‘Universal Health Coverage’.
Wakiongozwa na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, Magavana hao wamesema Serikali imeweka pengo kati yake na Serikali za Kaunti akisema hali hiyo itatatiza pakubwa sekta hiyo.
Kulingana na Joho bima ya kitaifa ya afya NHIF imezembea katika kushirikiana na Serikali za Kaunti hali inayofanya kaunti kugharamikia matibabu ya Wafanyikazi wake licha ya kukatwa fedha ili kuchangia hazina hiyo.
Joho amesema hazina hiyo inazikimu hospitali za kibinafsi kwa malipo hayo ilhali imejitenga na hospitali za umma, akisema kwamba hali hiyo italemaza kabisa mpango wa huduma ya afya kwa wote nchini.
Kauli ya Joho imeungwa mkono kikamilifu na Mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Wycliff Oparanya aliyesema kwamba bila ya Serikali kuwekeza zaidi katika mpango huo na kuzikimu Kaunti kwa fedha, mpango huo utasambaratika.
Magavana hao walikuwa wakiwasilisha matakwa yao kuhusu sekta ya afya kwa Waziri wa afya Mutahi Kagwe katika mkao uliyofanyika Mjini Mombasa.