Serikali kufanya juhudi kwa wanaotumia kivuko cha Feri cha Likoni kufuata maagizo ya kiafya dhidi ya Corona
Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha watumizi wa kivuko cha feri cha Likoni wanazingatia masharti ya kiafya ya kuzuia maambukizi ya Corona.
Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani John Elungata amekiri kuwa kivuko cha feri cha Likoni kinashuhudia msongamano mkubwa wa watu na magari na ni lazima mikakati iidhinishwe ili kuzuia maambukizi.
Elungata amesema kivuko hicho kinachowahudumia zaidi ya watu laki tatu na magari elfu 6 kila siku, kimekubwa na changamoto katika kuidhinisha mbinu za kuzuia maambukizi ya Corona.
Afisa huyo tawala amewataka wale wanaosimamia shughuli katika kivuko hicho kuhakikisha watumizi wanazingatia masharti ya afya na kuwazuilia wale watakaokosa kuvaa barakoa na kutumia kivuko hicho.