SHEPHERD AFUNGUKA KUHUSU PESA YA MCSK
Mwanamuziki Mohamed Mrisa maarufu kama Shepherd wa Shemakinz amefuguka kutolipwa na Music Copyright Society of Kenya, MCSK, hata baada ya rais wa jamuhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kugawiwa jumla ya shilingi milioni 200 kila mwezi kwa wanamuziki wote kutokana na kufutiliwa mbali kwa show za muziki kama njia mojawapo ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona.
Mwanamuziki huyo ambaye anajulikana kwa wimbo wake maarufu ‘Nifunge’ amethibitisha kuwa yeye ni mmoja kati ya wasanii ambao bado hawajalipwa licha ya kujisajili na MCSK mwaka wa 2014. Hata hivyo amedokeza kwamba MCSK bado wanaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba wasanii wote watalipwa.
Kupitia mahojiano ya simu na Radio Kaya, Shepherd ametaja wakati huu ambapo tunakabiliana na janga la Covid-19 kuwa kipindi kigumu hasa kwa wasanii ambao wanategemea muziki kama njia pekee ya kupata riziki zao. Aliongeza kuwa kutoa ngoma mpya muda huu ambapo kila mmoja anazungumzia janga hili la Corona kama kazi bure tu kwani kila mmoja ameelekeza akili na juudi zake kwa janga hilo.
Hata hivyo, Shepherd pia amefichua kuachia nyimbo yake mpya baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Hii ni baada ya kukaa kimya mwa muda mrefu sasa. Katika wimbo huo amemshirikisha mwanamuziki wa kike ambaye alikuwa chini ya usimamizi wa mwamba records, lakini sasa yupo chini ya usimamizi wake. Shepherd ametangaza kumzindua rasmi mwanamuziki huyo kwa mashabiki na kazi hiyo ambayo imetengezwa na Producer Tee hits.
Mwanamuziki huyo amesema kuwa uamuzi wake wakumshirikisha msanii huyo wa kike ni katika juhudi ya kuhamasisha wasanii wa jinsia ya kike katika kiwanda hiki.