Msimu wa Masika utakuwa na mvua nyingi wasema watabiri wa hali ya hewa
Mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo Afrika Mashariki na pembe Ya Afrika yatashuhudia viwango vya juu vya mvua na joto katika msimu wa miezi ya Machi, Aprili na Mei.
Akitoa mwelekeo wa msimu huo uliotolewa na shirika la kutabiri hali ya hewa la (ICPAC), Mkurugenzi mkuu wa idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Bi Stella Aura amesema kuwa maeneo ya magharibi, kusini magharibi mwa Kenya, Uganda Mashariki, Magharibi mwa Rwanda na Sudan Kusini yatapokea Mvua kubwa ambazo zinauwezo wa kusababisha mafuriko.
Bi Stella amezihimiza idara husika kuchukua tahadhari ya mapema ya kuepukana na majanga yatakayosababishwa na mvua ya msimu wa masika.
Kulingana na Mkurugenzi huyo mvua ya msimu wa vuli itaanza mapema katika maeneo ya kaskazini mwa Tanzania, Uganda, Magharibi na Kaskazini mwa Kenya, kusini Magaribi mwa Ethiopia na Somalia kusini.
Hata hivyo mvua itachelewa kunyesha katika maeneo ya kati na kaskazini mashariki mwa Ethiopia na kaskazini mwa Somalia huku viwango vya juu vya joto vikitatarajiwa katika nchi ya Eritrea na sehemu za mashariki mwa Somalia na Ethiopia.
Bi Stela aidha amezihimiza idara husika kuchukua hatua baada ya kupata utabiri wa hali ya hewa katika mipangilio yao ili uweze kumsaidia mwananchi wa kawaida.
Baada ya kutolewa kwa utabiri huu wa Mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo Afrika Mashariki na pembe Ya Afrika, nchi wanachama zinatarajiwa kutoa utabiri wa nchi zao ndani ya mwezi.