Wanaovamia malori ya uchukuzi waonywa
Wakaazi wa maeneo ya Samburu, Taru na Macknon road katika Gatuzi dogo la Kinango wameonywa dhidi ya kuyavamia magari katika barabara kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Jijini Nairobi na kuiba mizigo.
Kamanda mkuu wa polisi katika Ukanda wa Pwani Marcus Ocholla amesema madereva wanaotumia barabara hiyo kuu wakisafirisha shehena inayotoka katika bandari ya Mombasa mara kwa mara huvamiwa na mizigo hiyo kuibwa hasa nyakati za usiku.
Akizungumza baada ya kufanya vikao vya umma katika maeneo hayo, Ocholla amewataka Wakaazi hao kukomesha mara moja tabia hiyo ailiyoitaja kama hatari kwa maisha yao na inayowatishia wawekezaji vile vile.
Ocholla vile vile amewakosoa Wakaazi hao kwa kuyavamia matrela ya kusafirisha mafuta ya petroli na kuchota mafuta hayo au yale ya dizeli pindi magari hayo yanapokumbwa na hitilafu barabarani, akisema kwamba hatua hiyo ni hatari mno na Mafisa wa usalama watapambana na wezi hao.
Kamanda huyo wa polisi katika Ukanda wa Pwani ametaja wizi wa chakula kama vile mchele, maharagwe, sukari na ngano kutoka kwa malori kama uliyokithiri mno katika maeneo hayo.