Dama aolewa
Taarifa na Dominick Mwambui
Kwale, Kenya, Juni 30 – Vifijo na nderomo zilitanda mjini Kwale siku ya Jumamosi ya tarehe 29 mwezi wa Juni pale mtangazaji wa kipindi cha Voroni Enehu, Beatrice Dama Kahindi alipofunga pingu za maisha na mpenzi wake wa muda mrefu Victor Caleb katika harusi ya kifahari.
Mbele ya halaiki iliyojumuisha watu mashahuri wawili hao walilishana yamini katika ufuo wa hoteli ya Sanorisa ambapo karamu ya ndovu kumla mwanawe iliandaliwa.
Wanamziki mashuhuri , wafanyi biashara na wanasiasa ni miongoni mwa wale waliohudhuria karamu hiyo ambayo imesalia kuwa gumzo la wengi.
Mmiliki wa kituo cha Radio Kaya Bi Rose Mwakwere na mumewe Balozi Chirau Ali Mwakwere ni miongoni mwa wale waliohudhuria harusi hiyo ya kipekee.
Kwa upande wake Mkurungezi wa Radio Kaya Bi Rose Mwakwere, amewashauri Beatrice na Victor kuzidi kumcha mwenye Mungu ili azidi kuwaongoza katika maisha yao ya ndoa na kutafuta ushauri nasaha kwa marafiki wema kwani sasa wamekuwa kitu kimoja.
Dama ambaye pia ni Balozi wa utamaduni wa kimijikenda ameambia uhondo kuwa hafla hiyo ilifana kiasi cha kwamba alishindwa kuyazuia machozi yake.
“Imekuwa siku ya kufana sana na ambayo sitawahikuisahau maishani mwangu, kila nikifikiria ufanisi wa leo nashindwa kujizuia, natiririkwa na machozi ya furaha. Mume wangu amepata tabu yakunipangusa machozi tu,” amesema bibi harusi huyo kwa njia ya simu kutoka eneo la siri ambapo wapo fungate kwa sasa.
Kutoka kwa dawati la Uhondo tunawatakia wapenzi hawa wawili kila la kheri maishani.