Wakenya milioni 2.5 ni waraibu wa tumbaku
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reachout Centre Trust’ Taib Abdulrahman. Picha/ Reach Out Centre Trust
Taarifa na Alphalet Mwadime
Mombasa Kenya, Mei 31- Zaidi ya Wakenya milioni 2.5 humu nchini wamezama katika uraibu wa tumbaku.
Akiyafichua hayo katika kumbukumbu za siku ya kukabiliana na utumizi wa tumbaku mjini Mombasa, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reachout Centre Trust’ Taib Abdulrahman amesema utumizi wa tumbaku hasa uvutaji sigareti miongoni mwa vijana wadogo umekithiri katika ukanda huu.
Taib ameishinikiza Serikali kuweka sera na sheria mwafaka zitakazodhibiti utumizi wa tumbaku nchini, akisema uraibu huo umechangia maradhi mengi yanayofungamana na mapafu.
Mkereketwa huyo wa kupambana na uraibu wa dawa za kulevya nchini amehoji kuwa wengi wa waraibu huo wameanzia katika hatua ya sigareti na, akiutaja utumizi wa tumbaku kama uliyo na athari kubwa kiafya.