Picha kwa hisani –
Mwanamuziki wa Congo Tshala Muana amekamatwa na shirika la ujasusi la DRC kwa ajili ya wimbo wake mpya kwa jina Ingratitude unaoonekana kumkosoa rais wa sasa Felix Tshisekedi.
Producer wake Claude Mashala amethibitisha kukamatwa kwa mwanamuziki huyo kwa ajili ya maudhui
ya wimbo wake ambao haujawapendeza baadhi ya maafisa wakuu serikalini . Wimbo huo unamkosoa
mtu ambaye aliwasaliti watangulizi wake ukionekana kuashiria uhusiano mbaya wa sasa kati ya rais
Tshisekedi na mtanguzi wake Joseph Kabila.
Mwanamuziki mwenzake Lofombo Gode amesema ingawaje hakuna majina yaliotajwa katika wimbo
huo, inadaiwa una maana ya ndani ambayo haijawafurahisha wafuasi wa rais wa sasa.
Jamaa za mwanamuziki huyo maarufu wamesema alichukuliwa na maafisa wa ANR ili kuhojiwa na
wamelalamika kuhusu alivyokamatwa.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 62 ni mfuasi wa rais wa zamani Joseph Kabila kwani awali aliwahi
kuteuliwa kuwa mbunge na babake rais huyo marehemu Laurent Kabila.
Katika wimbo wa Tshala Muana ,waliofaulu kuunganoisha maana yake na hali ya sasa ya kisiasa
wanasema ,anayelaumiwa kwa kuwasaliti watangulizi wake ni rais Tshisekedi ambaye Kabila alimsaidia
kutengeza muungano wa kuunda serikali yake lakini kwa muda sasa uhusiano katika muungano huo
haujakuwa mzuri na kuzua taharuki katika taifa hilo.
Wafuasi wa Tshisekedi, kwa sasa hawapatani na kambi ya Kabila na wimbo huo unaonekana kumlenga
rais.
Serikali haijatoa maelezo kuhusu kukamatwa kwa Tshala Muana lakini imepiga marufuku kuchezwa kwa
wimbo huo huko Congo.