Picha kwa hisani
Maafisa wa polisi mapema leo wametibua maandamano yaliyolenga kumkashfu Katibu wa maswala ya ubaharia nchini Bi Nancy Karigithu aliyedai kwamba Vijana wa Ukanda wa Pwani wamekosa ajira katika sekta hiyo kutokana na ukosefu wa ufahamu wa lugha ya Kiingereza.
Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la ‘Sisters for Justice’ Bi Naillah Abdallah Vijana hao wamemtaka Karigithu kuomba msamaha na kujiuzulu mara moja kwenye wadhfa huo kutokana na matamshi hayo.
Naillah amesema vijana wa pwani wamesoma na wana tajriba ya juu japo wametengwa katika ugavi wa nafasi za ajira akimtaka Karigithu kutoa majina ya Vijana waliyoshindwa kuongea kwa Kiingereza walipokuwa wakitafuta ajira katika sekta ya ubaharia.
Mwanaharakati huyo wa kijamii amesema vijana hao wataandamana kila uchao ili kushinikiza kuhusishwa kikamilifu kwa vijana katika ugavi wa nafasi za ajira kwa jamii ya hapa Pwani.