Picha kwa Hisani –
Wakaazi wanaotumia kivuko cha feri cha Mtongwe wametatizika baada ya feri iliyokuwa ikihudumu katika kivuko hicho kuondolewa mapema leo.
Wakaazi hao waliyokua wamefika katika eneo hilo wamelazimika kurudi katika kivuko cha feri cha Likoni ili kuvuka kuelekea Kisiwani Mombasa.
Wakaazi hao wamelalamikia ukosefu wa mpangilio katika kivuko hicho huku wengi wakitumia kile cha Likoni wakidai kivuko hicho cha Mtongwe kimekuwa cha kubahatisha tangu kuzinduliwa tena takriban majuma mawili yaliyopita.
Hata hivyo, Shirika la huduma za feri nchini limesema feri hiyo imeondolewa na kupelekwa katika kivuko cha feri cha Likoni baada ya ile ya MV- Safari kukumbwa na hitilafu za kimitambo.
Usimamizi wa Shirika hilo la feri hata hivyo umesema kwamba huduma za feri za Mtongwe zitaregeshwa pale MV-Safari itakaporekebishwa.