Picha kwa Hisani –
Wizara ya Afya nchini imewahimiza wakenya kuwa waangalifu zaidi wakati huu msimu wa baridi na upepo mkali kutokana na mabadiliko ya anga ili kujikinga na maradhi mbalimbali.
Akitoa himizo hilo, Katibu mkuu msimamizi katika Wizara hiyo Dkt Rashid Aman, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuvaa sweta, barakao, kukaa umbali wa mita moja kutoka kwa mwengine sawia na kuzingatia masharti yote ya kiafya.
Akigusia takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona, Dkt Aman amesema watu 544 wamethibitishwa kupata maambukizi hayo kutokana na sampuli 2,653 na idadi hiyo kuongezeka hadi watu 22,597.
Dkt Aman amesema kati ya watu hao 544, wakenya ni 499 huku watu 45 wakiwa raia wa kigeni na wanaume ni 315 huku wanawake wakiwa 229 na wagonjwa hao wana umri wa kati ya mwaka mmoja na 84.
Hata hivyo amedokeza kuwa watu 263 wamepona virusi hivyo kwani wagonjwa 176 walikuwa wakihudumiwa nyumbani huku 87 wakihudumiwa katika hospitali mbalimbali nchini na sasa idadi watu waliopona Corona imefikiwa 8,740 huku watu 13 wakiaga dunia.