Picha kwa Hisani
Utata umezidi kuikumba kesi iliyowasilishwa mahakamani na watetezi wa haki za kibinadamu, kupinga mpango wa kuunganisha wakenya wa BBI.
Kulingana na Mwenyekiti wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la MUHURI Khelef Khalifa na Mwanaharakati Okiya Omutatah waliowasilisha kesi hiyo Mahakamani, wanadai kuwa majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo wote wamejiondoa.
Khalifa amesema hatua ya Majaji wa kitengo cha kikatiba na haki za kibindamu kujiondoa kwenye kesi hiyo ni wazi kuwa wametishiwa na wale wanaotetea mchakato huo wa BBI.
Khalifa sasa anataka gharama ya mchakato wa BBI kuwekwa wazi kwa wakenya na Serikali kueleza ilitumia mbinu gani katika kutenga fedha hizo ambazo bunge la kitaifa halikuhusishwa.
Kesi hiyo ambayo sasa imerudishwa kwa Jaji mkuu David Maraga ili kuteua Majaji wapya, imepitia mikoni mwa Jaji John Mativo, Weldon Korir, John Nyamweya, James Makau na Pauline Nyamweya ambao wote wamejiondoa katika kesi hiyo.