Mwanamuziki chipukizi kutoka Ukunda kaunti ya Kwale, Mohamed Mansuri Party maarufu kama Yuro Millionaire azuiliwa kuachia ngoma yake mpya ‘Basi Iwe’ na wazazi wa vixen wake wakidai kuwa hawakumpa ruhusa hiyo na kwamba hawakufurahishwa na mavazi yake kwenye video hiyo. Nyimbo hiyo ilikuwa iachiwe siku ya leo na msanii huyo na alikuwa amerecord video fupi na kuipost siku ya jana jioni akiwaelezea mashabiki wake kuwa video ya ngoma hiyo ingepatikana kwenye mtandao wa YouTube asubuhi ya leo.
Huu ni wimbo wa Yuro wa kwanza kuufanyia video, lakini ni wa tatu kurecord chini ya usimamizi wa Waghetto empire (WGT) baada ya nyimbo zake maarufu ‘Narira’ na ‘Maria’
Mashabiki wa mwanamuziki huyo wameamkia habari hiyo iliyo chapishwa kwa ukurasa wa producer Bang Belly kwenye akaunti yake ya Facebook ambaye alikuwa anawaomba radhi mashabiki wa Yuro kwa kutoachia muziki huo siku ya leo kama walivyokuwa wanatarajia. Akithibitisha taarifa hii, producer wa nyimbo hiyo, kupitia kwa njia ya simu na Radio Kaya, amesema kwamba alipokea simu asubuhi sana kutoka kwa Yuro, akimuelezea yaliyomsibu. Yuro alikujiwa nyumbani na wazazi wa msichana huyo wakiwa wame andamana na mzee wa mtaa na kumpeleka hadi kwa afisi ya chifu wa maeneo hayo ili kuweza kutatua shida hiyo.
“Jambo mashabiki wa Yuro na WGT, video hii ya Basi We by Yuro ilikuwa ni tuiachilie leo lakini kwa sababu zisizoepukika haitoachiliwa. Tunajua mmeisubiri kwa hamu ila tunawaomba msamaha na mtuvumilie tutatue shida iliopo. Kwa lolote lile tutawafahamisha kupitia mtandao na media zingine. Ila usisahau kusubscribe kwa channel yake ya YouTube tatizo tukilitatua uwe wa kwanza kuitazama.”
Kulingana na producer Bang Belly, msichana huyo ana umri wa zaidi ya miaka 18 na alijitokeza mwenyewe wakati walipokuwa wanatafuta video vixen wa muziki huo. Pia, wasimamizi wa Yuro ambao ni Waghetto empire walimlipa pesa ambazo walikuwa wamekubaliana hapo awali, baada ya kazi kukamilika. Wazazi wa mrembo huyo hivi sasa, wanadai kulipwa shilingi elfu hamsini la sivyo video hiyo isiwachiliwe. Bang Belly ameeleza kuwa japo kuwa silo jambo dogo lakini wanaendelea na mazungumzo na kwamba wana imani kubwa sana kuwa watalitatua mwisho wa siku ya leo.
Juhudi zetu za kumpata Yuro kupitia njia ya simu ziligonga mwamba, baada ya simu yake kushikwa na mwanamke mara ya kwanza kisha, jamaa aliyedai kuwa ndugu yake, tulipopiga mara ya pili. Ndugu yake Yuro hata hivyo pia alithibitisha kisa hicho akisema kuwa bado walikuwa wanaendelea kusuluhisha mzozo huo.
Wanamuziki wenzake pamoja na mashabiki wake wamekitaja kitendo hiki cha wazazi wake kutaka kulipwa hela kabla ya kuwachia nyimbo hiyo kama tamaa.
Sasa, haija bainika bado ni lini ngoma hiyo itawachiwa.