Msanii chipukizi aliyetamba kwa nyimbo yake ‘Narira’ Mohamed Mansuri Partty almaarufu kama Yuro Millionaire kutoka Ukunda katika kaunti ya Kwale ametajwa kama msanii chipukizi bora mkoani Pwani na wasanii wakongwe Ally B, Fat-S pamoja na Zikky Mtanah. Kupitia mahojiano ya moja kwa moja na Radio Kaya kwenye kipindi cha Kaya Flavaz, wanamziki hao wakongwe walimpongeza Yuro kwa juhudi na bidii zake kwenye sanaa ya muziki. Ziky alimsifu kwa utunzi wake huku Fat-S akimtia moyo kuwa atakuwa mwanamuziki maarufu sana na kazi yake kujulikana hata nchi jirani hivi karibuni.
Hii ni baada ya Yuro kutoa wimbo wake mpya kwa jina ‘Maria’ ikiwa ni ngoma yake ya pili baada ya ‘Narira’ ambayo ilifanya vyema kwenye chart ya Tano bora za saa tano kwenye kipindi hicho na pia kupigiwa kura ngoma ya pili bora zaidi mkoani Pwani ya mwaka wa 2019 baada ya ‘Sokote’ yake Masauti tarehe 01-01-2020.
Msanii Yuro Millionaire mwenye umri wa miaka 25, aliingia kwenye sanaa ya muziki mwaka wa 2015 kama mwanamuziki wa hiphop alipoimba ‘hiphop time’ chini ya usimamizi wa Bidi Badu lakini alibadili mtindo na kuimba Narira’ mwezi Octoba mwaka jana chini ya usimamizi wa Blue Star Records na ‘Maria’ mwezi wa January mwaka huu chini ya Waghetto Records. Nyimbo zake hizi mbili hata hivyo zimetengezwa na Producer Bang Belly.
Wakifanya mahojiano ya ana kwa ana na kituo kimoja cha redio mjini Mombasa, Meneja wake ambaye ni msanii na producer Bang Belly, alimsifia kwa upole wake na mwenye kujituma.
Je, unadhani kuwa Yuro ata fanikisha ndoto zake za kuwa mwanamuziki tajika ndani na nje ya nchi?